Monday, August 13, 2012

MBWANA SAMATTA NA TP MAZEMBE

CHANZO: SHAFFI DAUDA

MBWANA SAMATTA NA GARI LA MILLIONI 50 -MCHEZA SOKA WA KIBONGO ANAYELIPWA FEDHA NDEFU ZAIDI


Akiwa ndio mchezaji aliyesajiliwa kwa fedha ndefu kutoka nchini Tanzania, Mbwana Ally Samatta anaishi ambayo mcheza soka wa kimataifa anastahili kuishi.

Akiwa ameuzwa kwa dola za kimarekani zaidi ya 100,000, kwenda TP Mazembe kutoka Simba, Mbwana Samatta analipwa kiasi cha dola 5000 kwa mwezi ambayo ni sawa na shilingi millioni 7.5 huku akichukua marupurupu ya kutosha.

Mbwana Samatta amekuwa akicheza na kuperfom kwa kiwango kikubwa katika kila nafasi anayopata anapoichezea klabu yake na kwa kiwango alichoonyesha kuna uwezekano mkubwa mkataba wake utaboreshwa zaidi na kuendelea kuvuna mkwanja mrefu zaidi.


Kwa sasa hivi Samatta amenunua gari la kisasa zaidi Chrysler Crossfire la mwaka 2006 ambalo limemgharimu takribani millioni 50 za kibongo.

Ikiwa Samatta ataendelea kucheza kiwango alichonacho sasa, basi ni dhahiri tutaendelea kuona akiishi kwenye majumba ya kifahari huku akipush magari ya gharama.

MICHEZO-KIMATAIFA

 

CHANZO: SHAFFIH DAUDA

MAREKANI YAONGOZA KWA MEDALI NYINGI OLIMPIKI, CHINA YAFUATIA, UINGEREZA NAO KIFUA MBELE

Wachezaji wa timu ya mpira wa kikapu ya Marekani wakiwa na medali zao za dhahabu.

Pata habari za michezo. Bonyeza link hapo chini.

www.shaffihdauda.com

Pata habarikutoka idhaa ya kiswahili ya BBC

www.bbc.co.uk/swahili

MICHEZO-KITAIFA

Yanga yatete kombe la Kagame
Jumatatu, 30 Julai 2012 10:40
MABAO yaliyofungwa na Hamis Kiiza na Said Bahanuzi yameipa ubingwa wa mara tano Yanga wa Kombe la Kagame.
Kwa ushindi huo Yanga ambao walikuwa mabingwa watetezi wamefanikiwa kutetea ubingwa wao, huo kwa mara nyingine tena.
Mchezo huo ambao ulitawaliwa na vituko vingi kabla ya kuanza nahodha wa Azam, Agrey Morris alikataa kupeana mikono na mwenzake wa Yanga, Nadir Haroub.
Mchezo huo ulianza kwa kasi huku Azam wakionekana kutaka kupata bao la mapema, ambapo iliwachukua dakika mbili kabla ya John Boko kulifikia lango la Yanga lakini alipiga shuti lilotoka nje.
Dakika 12 baadae, Kipre Tchetche kama angekuwa makini angeweza kuipatia Azam bao la kuongoza.
Azam waliendelea kulisakama lango la Yanga ambapo dakika ya 15 walipata kona iliyopigwa na Abubakar Salum na kuungwanishwa na Moris kwa kichwa na mpira kumgonga Ally Mustapha.
Yanga walijibu shambulizi hilo kwa Haruna Niyonzima kuwalamba chenga mabeki wa Yanga na kupiga krosi safi iliyookolewa kiufundi na Deogratius Munishi.
Baada ya kuona mashambulizi yamezidi kocha wa Yanga, Tom Sainttief alimuita Niyonzima na kumweleza kitu ambapo baada ya hapo ‘alijiungashusha’ na kujidai ameaumia huku kocha huyo akitumia muda huo kuwaita wengine na kuwapa maelekezo.
Azam walitawala kabisa mchezo huo kwa dakika 30 za mwanzo huku wenzao wa Yanga wakipoteana kabisa.
Dakika 30 Bahanuzi alifanikiwa kuwalamba chenga mabeki wa Azam ndani ya eneo la hatari lakini alitoa pasi ambayo ilitoka nje.
Rashid Gumbo alipiga shuti kali dakika ya 34 ambalo lilitemwa na Munishi na kumkuta Bahanuzi ambaye alipiga nje.
Uzembe uliofanywa na Agrey Moris kwa kumudishia mpira mfupi Munishi ambao uliwahiwa na Kiiza aliyepiga shuti na kumgonga kipa na kujaa wavuni.
Kipindi cha pili kilianza kwa David Luhende kuwalamba chenga wachezaji wa Azam na kumpa pasi safi Gumbo ambaye alipiga shuti lilodakwa na Munishi.
Yanga ambao walionekana kupata nguvu zaidi kipindi cha pili, waliendelea kulisakama lango la wapinzani wao.
Kama Kiiza na Niyonzima wangekuwa makini wangeweza kuipatia Yanga mabao dakika za 58, 82 na 86.
Mabeki wa Azam watajutia makoa waliyofanya katika mchezo huo ambapo walitegeana kuokoa mpira ambao uliwahiwa na Bahanuzi na kuachia shuti kali lilojaa wavuni na kuipatia Yanga bao la pili.
Kikosi: Ally Mustapha, Nadir Haroub, Stephano Mwasika, Kelvin Yondani, David Luhende, Athuman Iddy, Rashid Gumbo/Juma Seif, Oscar Joshua, Hamis Kiiza, Said Bahanuzi na Haruna Niyonzima.
Azam FC: Deogratiu Munishi, Ibrahim Shikanda, Said Morad, Erasto Nyoni, Aggey Moris, Jabir Aziz/George Odhiambo, Kipre Tchetche/Mrisho Ngasa, Salum Abukar, John Boko, Ibrahim Mwaipopo na Ramadhani Chombo.
Baada ya mchezo huo kocha mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema kikosi chake kimecheza vizuri huku akitoa sifa nyingi kwa kiungo wake chipukizi Abubakar Salum.
Alisema kikosi hicho hakitabadilika katika ligi kuu msimu ujao na kuwaongezea mazoezi kwa ajili ya ligi hiyo.
Pia aliongeza kuwa John Boko ameshindwa kufanya vile ambavyo alitegemea baada ya kucheza katika kiwango cha chini.
Alisema kupoteza mchezo huo kumetokana na kutotumia nafasi ambazo walipata huku wapinzani wao wakizitumia.
Kwa upande wake kocha wa Yanga alisema Tom Saintfiet alisema anashukuru ameanza vizuri katika timu hiyo kwa kunyakuwa kombe la kwanza.
Alisema timu ya Azam ni kati ya timu bora ambayo ina viungo wengi wazuri, ambapo kama itatunzwa itakuja kuwa bora zaidi baadae kutokana na kuwa na wachezaji wengi vijana.
Alisema anawashukuru wachezaji wake kwa kufuata maagizo yake japokuwa ailikuwa katika kipindi kifupi toka alipojiunga na timu hiyo.
Wakati huo huo Said Bhanuzibaliyesajiliwa na timu hiyo alitokea Yanga amefanikiwa kuibuka mfungaji bora wa michuano hiyo kwa kufunga mabao sita.
Kutokana na kunyakuwa ubingwa huo Yanga imefanikiwa kupata kitita cha dola 30,000, Azam walioshika nafasi ya pili wamepata dola 20,000 huku Vita ya Kongo DRC iliyoshika ya tatu ikipata dola 10,000.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji alionekana ntu mwenye furaha kubwa kuliko mwingine yoyote katika matokeo hayo.
Manji ambaye aliapa ataifanyia kweli Azam kabla ya mchezo huo, alionekana mwenye furaha kubwa wakati wote huku akicheza wakati mwingi wa mchezo.
“Achana na Manji, yaani kama kuna kitu kimemfurahisha ni leo,” alisema shabiki mmoja.
Naye mshambuliaji Said Bahanuzi, aliwakosha zaidi mashabiki wa Yanga kutokana na kufunga bao hilo katika dakika za nyongeza.

Sunday, August 12, 2012

Zitto ataka kampuni isipewe leseni kuchumba urani

HABARI KUTOKA GAZETI LA MWANANCHI
Na :-Daniel Mjema, Dodoma
Zitto ataka kampuni isipewe leseni kuchumba urani

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto ameitaka Serikali kutoipatia leseni ya uchimbaji wa madini ya urani, kampuni ya Uhuru One hadi iilipe Serikali kodi ya Sh297 bilioni.

Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, alitoa pendekezo hilo bungeni mjini Dodoma jana aliposimama na kutumia kanuni ya 68(1) kueleza kutoridhishwa na majibu ya Serikali kwenye swali la 353.

Katika swali hilo, Mbunge wa Jimbo la Mkoani, Ali Khamis Seif (CUF), alitaka kufahamu Serikali itanufaika vipi na uchimbaji wa urani utakaoanza mwakani katika hifadhi ya Selous.

Katika majibu yake, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema uchimbaji wa madini hayo utailipa Serikali
mrabaha wa asilimia tano ya urani yote itakayozalishwa.

Pia alisema Serikali itashiriki katika miradi ya urani kwa kuwa na hisa bila kuwekeza mtaji wowote na kupata gawio kama mwana hisa,
achilia mbali kodi mbalimbali itakazolipwa.

Hata hivyo, Zitto alisema baada ya Kampuni ya Mantra ya Australia kukamilisha kazi ya utafiti wa urani, iliuzwa kwa kampuni ya Urusi
inayojulikana kama ARZM kwa Dola za Marekani 980 milioni.

Alisema baada ya mauzo hayo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) , walitaka walipwe asilimia 20 kama kodi ambayo ni Dola 186 milioni za Marekani, sawa na Sh297 bilioni.

“Uhuru One inayotaka kuchimba madini hayo ya Urani ni kampuni tanzu ya ARZM ya Urusi tutasikitika sana kama leseni ya uchimbaji itatolewa kabla ya kulipwa kwa kodi hiyo,” alisema.

Hata hivyo, katika maelezo yake hayo, Zitto hakufafanua sababu za fedha hizo kutolipwa hadi sasa lakini alisisitiza kuwa ni vyema
Serikali isitoe leseni ya uchimbaji hadi zilipwe.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema, Serikali inafahamu zaidi kuhusu jambo hilo na kwamba
leseni haijatolewa na haitatolewa.

Papaa Msofe kizimbani kwa mauaji Dar

Papaa Msofe kizimbani kwa mauaji Dar

MFANYABIASHARA wa Dar es Salaam, Abubakar Marijani (50) maarufu kwa jina la Papaa Msofe amepandishwa kizimbani akikabiliwa na shtaka la mauaji.
Papaa Msofe alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Akimsomea shtaka hilo, Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka alidai kuwa Novemba 6, 2011, mshtakiwa alimuua mfanyabiashara wa madini, Onesphory Kituli.

Tumaini alidai kuwa mauaji hayo aliyafanya nyumbani kwa marehemu Magomeni Mapipa, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Wakili Kweka alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume cha Kifungu cha 196 cha Kanuni za Adhabu, Sura ya 19 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002.

Hata hivyo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo inatazamiwa kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa baada ya upelelezi kukamilika.
“Mshtakiwa hutakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hii haina uwezo wa kusikiliza mashauri ya mauaji,” alisema Hakimu wa Mahakama hiyo, Agnes Mchome baada ya Wakili Kweka kumaliza kumsomea shtaka hilo.

Wakili Kweka alisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na akaiomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Mchome aliamuru mshtakiwa arudishwe mahabusu hadi Agosti 23, mwaka huu wakati kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo kwa kuwa shtaka linalomkabili halina dhamana.

Papaa Msofe alifikishwa mahakamani hapo jana saa 3:30 asubuhi kwa kutumia gari la Polisi aina ya Toyota Land Cruiser akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi watatu, wawili kati yao wakiwa na silaha. Kwa siku kadhaa, mfanyabiashara huyo alikuwa akishikiliwa katika Kituo cha Polisi Magomeni.